METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 12, 2025

SERIKALI YAJIDHATITI KUIMARISHA USTAWI WA JAMII.



 Na Jackline Minja MJJWM , Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita, inaendelea kuweka kipaumbele katika ajenda ya ustawi na mifumo ya ulinzi wa mtoto, kuendeleza huduma za malezi mbadala, usimamizi wa Makao ya Watoto nchini ili kuhakikisha yanatoa huduma kwa viwango vinavyotakiwa.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa ziara ya kutembelea Makao ya Watoto ya Taifa Kikombo Jijini Dodoma na kujionea huduma zinazotolewa katika Makao hayo.


Mhe. Maryprisca amesema Makao ya Taifa ya Kikombo ni mfano wa Taasisi ya Serikali inayotekeleza majukumu hayo kwa weledi, upendo na dhamira ya dhati.


“Nimetembelea miradi, miundombinu na kupokea taarifa ya mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji kuimarishwa, nafurahishwa kuona jitihada kubwa zinazofanywa katika kutoa huduma ya Elimu, Afya, Lishe, ushauri nasaha pamoja na malezi kwa Watoto napenda kuwahakikishia kuwa Wizara itahakikisha Makao haya yanawezeshwa ipasavyo”. amesema Mhe. Maryprisca.


Aidha Mhe. Maryprisca ametoa rai kwa wadau wa maendeleo, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na jamii kuendelea kushirikiana na Wizara kwa kuwapa watoto fursa sawa za maendeleo kama ilivyo kwa watoto wengine wote wa Tanzania.


“Niwaombe Mashirika, wadau wa maendeleo tuendelee kuiunga mkono Serikali katika kuendeleza makazi ya watoto ili wawe na huduma nzuri na wasijione wanyonge na niwaambie kuwa ninyi ni watu muhimu, mnapendwa na Taifa linawahitaji, msipoteze matumaini, someni kwa bidii, zingatieni maadili, muwe na nidhamu na mtumie fursa mnazopata ili mkafikie ndoto zenu."

amesema Mhe Maryprisca


Katika hatua nyingine Mhe. Maryprisca ameupongeza Uongozi wa Makao ya Taifa ya Kikombo kwa kazi wanayoifanya na kuwataka kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha kuwa kila mtoto analelewa katika mazingira salama, yenye upendo na yenye kumjenga.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema watumishi wa Makao hayo wana weledi na uwezo mkubwa wa kutambua uwezo wa watoto licha ya changamoto wanazokuja nazo watoto katika makazi hayo.


“Hawa watumishi unaowona hapa wanauwezo wa kukaa nao, kuongea nao kwa mbinu tofauti ndio maana nasema hawa sio watu wakawaida hata mimi wakiniangalia wanasema hapo hauko sawa, lakini ni miongoni mwa watu walioaminiwa na Serikali ambao watatusaidia kukiendeleza Makao haya”. amesema Wakili Mpanju.


Awali akisoma taarifa ya huduma zinazotolewa katika makao ya Taifa ya watoto kikombo Afisa Ustawi wa Jamii Anord Fyataga amesema hadi sasa kituo kimepata mafanikio mengi ikiwemo kuimarika kwa huduma za ushauri na unasihi ambapo kila mtoto anapata ushauri wa moja kwa moja au wa makundi ,kuunganisha watoto 20 na familia zao, kuboreshwa kwa huduma za elimu ndani na nje ya makao ambapo wastani wa ufaulu wa watoto kwa shule za msingi na sekondari umeongezeka kwa asilimia mbili (2%) pamoja na kuwajengea ujuzi watoto 40 katika ujifunzaji wa stadi mbalimbali za maisha makaoni kama ushonaji wa nguo kwa kutumia cherehani.





Share:

WAZIRI WA ARDHI AWAASA WAHITIMU ARIMO KUJIEPUSHA NA MATENDO MAOVU


Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO

 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amewaasa wahitimu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kujiepusha na matendo maovu na elimu na maarifa waliyopata yawe tunu na faida kwa Taifa.


Mhe. Dkt Akwilapo ametoa wito huo tarehe 12 Desemba 2025 wakati wa mahafali ya 44 ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) yaliyofanyika mkoani Morogoro ambapo jumla ya wahitimu 450 wa fani za Jiomatikia (Upimaji Ardhi), Upangaji Miji na Vijiji na Mifumo ya Taarifa za Kijiografia (GIS) walitunukiwa Astashada na Stashahada katika fani hizo.


Mhe. Dkt Akwilapo amewataka wahitimu hao kukumbuka kuwa utii, nidhamu na tabia njema ni silaha itakayowafanya wapendwe mahali popote.


‘’Tukiwa hapa Morogoro tunakumbuka maneno yaliyoimbwa na mwanamuziki wa hapa hayati Mbaraka Mwinshehe na bendi yake ya Okestra Volcano; alisema “Heshima Kijana tanguliza kwanza mbele, ujeuri mbaya; uzuri si hoja tabia njema ni silaha utapendwa popote” mwisho wa kunukuu, alisema Mhe. Dkt Akwilapo.


Amewataka vijana kutodanganyika na maneno ya eti kuna watu wanaitwa Gen Z ambapo alieleza kuwa, hizo ni propaganda za kujenga hofu na kufifisha juhudi za nchi maskini kujitafutia maendeleo.


“Msidanganywe kuwa eti nyie ni kizazi cha vijana wasio na nidhamu, wapenda fujo, wasiosikiliza wazee wao, viongozi wao, chenye kujiamulia mambo yao bila kufuata sheria, taratibu, miongozo na tamaduni zetu; na mambo mengine ya hovyo’’ amesisitiza Mhe. Dkt Akwilapo.


Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inasikitisha na kushangaza kuona vijana wa Kitanzania wanasikiliza maelekezo ya watu ambao hawaishi Tanzania na wala hawajawahi kuwaona na kupuuza maelekezo ya Viongozi wao na hata wazazi wao ambao wamewalea mpaka hapo walipoifikia.


Amesema, kuhitimu masomo kunatakiwa kuendane na uzalendo waliojengewa wa kuipenda Tanzania na kusisitiza kuwa waithamini nchi yao.


Mhe. Dkt Akwilapo amewataka kutumia utaalamu walioupata kwa weledi, uadilifu na kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo na kuepuka vitendo vinavyoenda kuhatarisha amani.


Vile vile amewataka kuendelea kujifunza kwani elimu ni bahari, haina mwisho na kuwataka wanaobaki chuoni kuongeza bidii katika masomo, nidhamu na kutunza amani na umoja kwani kesho yao inajengwa na maamuzi ya leo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Bw. Musa Ramadhani Kilakala akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Adam Malima amesema, migogoro ya ardhi imepungua mkoani humo hasa pale wizara ya ardhi ilipoanzisha Kliniki za Ardhi ambazo amezieleza zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuwafikia wananchi katika maeneo yao.

Akitoa taarifa kwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Charles Saguda amesema chuo hicho kina Mpango Kabambe wa Miaka 20 (2023-2043) unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia na utendaji wa chuo katika kuwaandaa wataalamu wa sekta ya ardhi.

“Mpango kabambe huu unalenga kuongeza udahili wa wana chuo kutoka 660 hadi 5000, kuongeza watumishi kutoka 58 hadi 310 kuongeza program za mafunzo ya wanafunzi kutoka 2 hadi 7 pamoja na kujenga kampasi mpya katika eneo Mlima Kola mkoani Morogoro’’. Amesema Bw. Saguda.





Share:

Thursday, December 11, 2025

JENISTA MHAGAMA AFARIKI DUNIA

 

Dodoma, Tanzania - Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb), ametangaza kwa masikitiko makubwa kifo cha Mbunge wa Peramiho, Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, kilichotokea tarehe 11 Desemba, 2025 Jijini Dodoma.


Katika taarifa yake, Spika Zungu ametoa pole kwa Waheshimiwa Wabunge wote, familia ya marehemu, ndugu, jamaa pamoja na Wananchi wa Jimbo la Peramiho. Ameeleza kuwa ni kipindi kigumu kwa wote waliomfahamu na kushirikiana na marehemu, na amewaombea moyo wa uvumilivu na subira.


“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kilichotokea leo 11 Desemba, 2025 Jijini Dodoma. Natoa pole kwa Waheshimiwa Wabunge wote, familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na Wananchi wa Jimbo la Peramiho, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Spika Zungu 



Share:

Sunday, December 7, 2025

BMH YASOGEZA HUDUMA ZA AFYA KARIBU NA WANANCHI, YAHAMASISHA UCHANGIAJI DAMU, MSALATO MNADANI - KATIKA KUADHIMISHA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA.

 

Na Meleka Kulwa- Dodoma 

Desemba 6, 2025 Jijini Dodoma 

‎Hospitali ya Benjamin Mkapa imepeleka huduma za afya katika Viwanja vya Mnadani Msalato jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto yanayoadhimishwa kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka, kwa lengo la kuwafikia wananchi wasiopata kwa urahisi huduma za afya.

‎Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Bw. Teophory Mbilinyi, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amewahimiza wananchi wa Msalato na Watanzania wenye changamoto za kiafya kufika hospitalini  kwa matibabu ya kina ya huduma za kibingwa, akisisitiza kuwa kwa pamoja watajenga taifa.

‎Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Wauguzi, Bi. Mwanaidi Makao; aliwasisitiza wananchi kufika katika banda hilo ili kujipatia huduma mbalimbali zinazopatikana hapo, na aliahidi timu ya BMH itarudi katika awamu zingine katika kutoa elimu na huduma katika eneo hilo.

‎Pia kabla ya hapo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Ubunifu na Mratibu wa Huduma za Masuala ya Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto, Bi. Hindu Ibrahim, amesema kuwa timu ya madaktari, na wataalamu wengine imefika Msalato Mnadani kutoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi, hawakufika kwa ajili ya kutoa elimu pekee bali pia kutoa huduma za vitendo ikiwemo upimaji wa afya, uchangiaji damu na huduma za afya ya akili.

‎Bi. Hindu amesema kuwa Msalato Mnadani ni eneo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu wanaofika kwa shughuli mwisho wa wiki; baadhi hukosa muda wa kufika hospitalini. Kusogeza huduma katika eneo hilo kumewezesha kuwafikia wananchi ambao hawajapima afya kwa muda mrefu.

‎Baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo, akiwemo Ratifa Abdalah mkazi wa Miyuji, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili uokoa maisha ya watanzania Wenye matatizo na uhitaji wa damu. Aidha, amesema kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa inatoa huduma bora.

‎Kwa upande wake, Bi.Sauda Omary mkazi wa Msalato amesema kuwa  wananchi wanapaswa kupima afya na kujua hali zao. Akibainisha kuwa huduma zilizofikishwa Msalato ni msaada mkubwa kwa kuwa zimewasogezea huduma wananchi waliokuwa wakipata ugumu wa kufika hospitalini. aidha, Aliishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuendelea kusogeza huduma karibu na jamii.










Share:

Tuesday, December 2, 2025

BASHUNGWA: NINA MUDA WA ZIADA KUWAHUDUMIA WANANCHI WA KARAGWE.

 

Na Mwandishi Wetu- Karagwe 


‎📌 Baraza la Madiwani kupitia upya tozo kandamizi kwa Wakulima.

‎Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Karagwe kuwa ataendelea kushirikiana kwa ukaribu na Madiwani katika kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na kutatua changamoto na mahitaji ya wananchi ambapo ameeleza kuwa kipindi hiki kinampa nafasi na muda mpana zaidi wa kuwatumikia kwa ufanisi kama mwakilishi wao ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‎ Ameitoa kauli hiyo leo, tarehe 2 Desemba 2025, katika kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, kikao kilichohusisha viapo vya madiwani pamoja na uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri.

‎Bashungwa amesema kuwa katika kipindi hiki ameendelea kuboresha Ofisi ya Mbunge ili kuwasogelea na kuwahudumia wananchi kwa ukaribu zaidi ambapo atafungua ofisi mbili ndogo za Mbunge katika maeneo ya Rwambaizi na Nyaishozi, na tayari amenunua magari mawili aina ya “pickup” kwa ajili ya kuimarisha huduma kwa wananchi.

‎“Kipindi hiki ambacho nimepata muda wa ziada, niwahakikishie Wanakaragwe, kazi hii ya Ubunge niliiomba kutoka kwenu, mkaniamini na mnaendelea kuniamini. Nitatumia muda huu, hata kama ni kutembea kwa miguu au kwa njia yoyote ile, kufika kwenye vitongoji na vijiji vyote kuhakikisha tunasimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi,” amesisitiza Bashungwa.

‎Bashungwa amesema watashughulikia kero ya tozo kandamizi zinazowaumiza wakulima wanapopeleka mazao yao kwenye masoko na magulio kwa kushirikiana na Madiwani kuhakikisha zinapitiwa upya na kufanyiwa maboresho, sambamba na kuisimamia Halmashauri kufanya marekebisho ya kanuni ili kuondoa vikwazo vinavyowanyima wananchi tija na ustawi katika shughuli zao.

‎Aidha, Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani aliyomwonyesha katika kipindi kilichopita kwa kumpatia majukumu mbalimbali ya kuwatumikia Watanzania katika Serikali ya Awamu ya Sita.

‎Pia, amewashukuru wananchi wa Wilaya ya Karagwe kwa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge pamoja na Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

‎Akizungumzia miradi ya maendeleo, Bashungwa amesema ataendelea kushirikiana na Madiwani kusimamia kikamilifu miradi inayoendelea na ile mipya itakayoanza kutekelezwa katika Wilaya ya Karagwe, ikiwemo ujenzi wa Soko la Kisasa Kayanga na ujenzi wa stendi mpya ya Kishao.

‎Katika hatua nyingine, Bashungwa amewapongeza Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Longino W. Rwenduru (Diwani wa Kata ya Chanika), pamoja na Makamu Mwenyekiti, Adriani R. Kobushoke (Diwani wa Kata ya Rugu), kwa kuchaguliwa kwa asilimia mia moja kuongoza Baraza la Madiwani.






Share:

Saturday, November 29, 2025

MHE. NDEJEMBI AWAHAKIKISHIA WAKAZI WA KIGAMBONI UMEME WA UHAKIKA


 ‎📌Afanya Ziara katika Kituo cha Dege 

‎📌Aelekeza hatua za haraka kuchukuliwa kunusuru hali ya umeme Kigamboni

‎📌Umeme wa Megawati 22 kupatikana kwa hatua za haraka 

‎📌Upanuzi wa Kituo cha Dege wafikia asilimia 60 

‎Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya ziara ya kikazi ndani ya Mkoa wa kitanesco wa Kigamboni na kuagiza kuchukuliwa hatua za haraka za kuhakikisha hali ya umeme katika Mkoa wa Kigamboni inaboreshwa na kuwapa wakazi wa eneo hilo huduma ya uhakika alipotembelea Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza umeme cha Dege tarehe 29 Novemba, 2025.

‎“Leo tumekuja kuona ni namna gani Shirika letu la TANESCO linaweza kutatua changamoto hii kwa haraka zaidi na wameweka mipango mizuri ya muda mrefu katika kuhakikisha wanawezesha kupatikana kwa umeme wa uhakika kwa kujenga na kukiongezea nguvu Kituo cha Dege kwa kuweka transfoma ya MVA 120”, ameeleza Mhe. Ndejembi. 

‎Ili kukabiliana na changamoto ya huduma ya umeme iliyopo kwa haraka, Shirika limekuja na suluhisho la haraka kwa kujenga laini itakayosafirisha umeme kutoka Kituo cha Mbagala wa Megawati 22 kuja Kigamboni kuongeza upatikanaji wa umeme kwa Wananchi wa Kigamboni.

‎“Kwa hatua za haraka TANESCO wamenihakikishia kwamba kuna laini ya umeme ambayo italeta Megawati 22 kutoka Mbagala kuja Kigamboni ili kuongeza upatikanaji wa umeme kwa wakazi wa Kigamboni”, ameongeza Mhe. Ndejembi.

‎Sambamba na mikakati ya muda mrefu ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya umeme TANESCO imechukua hatua za haraka kunusuru kadhia hiyo kwa kuweka transfoma 93 ili kuondoa changamoto ya umeme mdogo pamoja na uzoezi la usimikaji wa transfoma 50 ambazo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, 2026 zitakuwa zimekamilika na kupunguza athari za kukosa umeme mara kwa mara.

‎“Kwa sasa ili kuondokana na changamoto hii, TANESCO imeanza kuweka transfoma kwa ajili ya kuondokana na hali ya umeme mdogo na pia wanaongeza transfoma zingine 50 kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme ambapo hadi kufika mwishoni mwa mwezi Machi,2026 zitakuwa zimekamilika kufungwa”, aliongeza. ‎

‎Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Mikaya Dalmia amemshukuru Waziri wa Nishati kwa kufanya ziara yake katika Wilaya hiyo na kuelekeza Shirika kutekeleza kwa haraka juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa umeme katika wilaya hiyo na kumuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa TANESCO kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya umeme. ‎

‎“Nitoe shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa ziara yenye matokeo chanya katika Wilaya yetu ya Kigamboni. Nikuahidi kuwa nitaendelea kushirikiana kwa karibu na wenzetu wa TANESCO katika kuwahudumia wananchi wa Kigamboni na kuhakikisha wanapata huduma bora ya umeme na pia nawasihi wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati changamoto hizi zinafanyiwa kazi na Shirika”, alieleza Mhe. Mikaya‎

‎Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji Umeme wa TANESCO Mha. Athanasius Nangali amemhakikishia Waziri wa Nishati kuwa kama Shirika wataendelea kufanyia kazi maelekezo yake na kuwa hatua za kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme ndani ya Mkoa wa Kigamboni zinaanza mara moja ili kuimarisha huduma hiyo. ‎

‎“Kama Shirika tutahakikisha kuwa tunafanyia kazi mara moja maelekezo tuliyopewa leo kwa kufunga transfoma na kuleta Megawati 22 Kigamboni kutoka mikoa ya Jirani ili kuimarisha hali ya umeme ndani ya Kigamboni”, alieleza Mha. Nangali.‎

‎Ziara ya Mhe. Ndejembi imelenga kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ndani ya Wilaya hiyo ikiwemo upanuzi wa Kituo cha Dege ambacho kukamilika kwake kutaipa Kigamboni umeme wa kutosha kuendesha shughuli za kiuchumi na kijamii.




Share:

MKUU WA MKOA SIMIYU AIPONGEZA SERIKALI KWA KUREJESHA AMANI, ATOA WITO WA KUIMALISHA UMOJA

 

Na Carlos Claudio, Dodoma.

‎Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na uongozi mzima wa serikali kwa kuhakikisha amani na kudhibiti vurugu zilizojitokeza mara baada ya uchaguzi.

‎Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya Mat Builders & Contractors, Mhe. Macha amewataka wananchi wa Simiyu na watanzania kwa ujumla kuendeleza utamaduni wa kulinda amani—nguzo muhimu inayowezesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

‎Akiwashukuru waandaaji na washiriki wa maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa amesema amefanikiwa kutembelea mabanda yote na kujionea ubunifu, teknolojia na kazi kubwa zinazofanywa na makampuni na taasisi mbalimbali.

‎“Nilipopata habari za maonesho haya niliona kuna fursa, na kama mtendaji mkuu wa mkoa sikuwa tayari kuikosa. Nimetembelea mabanda yote na nimebeba mambo mengi ya kwenda kuyafanyia kazi Simiyu,”alisema.

‎Amesema maonesho hayo yamedhihirisha kuwepo kwa teknolojia na ubunifu ambao unaweza kuongeza tija katika sekta za kilimo, ufugaji, ujenzi na viwanda—sekta muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Simiyu.

‎Mhe. Macha alibainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia, Mkoa wa Simiyu umepiga hatua kubwa, ukiwemo ujenzi wa barabara za lami zinazoziunganisha wilaya na mikoa jirani kama Mara, Mwanza na Shinyanga.

‎Akitaja baadhi ya miradi mikubwa, amesema mkoa unaendelea kunufaika na mradi wa maji wa shilingi bilioni 400 kutoka Ziwa Victoria unaohudumia wilaya za Busega, Bariadi, Ntilima hadi Maswa, ukitarajiwa kumaliza kabisa changamoto ya maji.

‎Aidha, mkoa upo katika hatua za mwisho kupata kituo kikubwa cha kupoozea umeme, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi upatikanaji wa nishati katika maeneo yote, ikiwa ni pamoja na vijiji.

‎“Ukiona eneo lina huduma zote za uhakika, basi jua hapo pana fursa za kiuchumi. Simiyu tunazipata huduma hizo, na uchumi wetu unazidi kukua,” alisema.

‎Mkoa wa Simiyu umeendelea kuwa kitovu cha kilimo cha mazao muhimu kama mpunga, dengu, choroko na hasa pamba, ambayo inalimiwa kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko mikoa mingine nchini. Pia, viwanda vingi vya kuchakata pamba vimejengwa mkoani humo, hatua inayoongeza thamani ya zao hilo.

‎Katika sekta ya ufugaji, Simiyu ina mifugo mingi ikiwemo ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku, hivyo teknolojia na mafunzo yanayotokana na maonesho kama hayo yanatazamwa kuwa kichocheo cha kuongeza tija kwa wafugaji na wakulima.

‎Mhe. Macha amesisitiza kuwa mafanikio yote yanayoonekana nchini hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani, akiwataka wananchi kutunza umoja na kutokurudia makosa ya nyuma.

‎“Kwa kweli haya tunayoona yasingewezekana bila amani. Tuishukuru serikali yetu, tuwashukuru viongozi wetu wakiongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha utulivu baada ya vurugu zilizojitokeza. Naomba wananchi wetu tujue yaliyoisha hatupendi yarudi tena.”

‎Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa anaamini maonesho ya Mat Builders & Contractors yakiletwa Simiyu yataongeza fursa mpya kwa wakulima, wafugaji na wawekezaji kutokana na teknolojia na huduma walizoziona.









Share:

Tuesday, August 5, 2025

TPHPA Yadhibiti Kweleakwelea kwa Mafanikio, Yaweka Mkakati wa Kilimo Salama kwa 2030

 





Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeongeza jitihada katika kudhibiti uvamizi wa visumbufu hatarishi, ikiwemo kweleakwelea, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha kilimo na kutekeleza Agenda 10/30   mpango wa kitaifa unaolenga kuongeza tija na ustawi katika sekta ya kilimo hadi kufikia mwaka 2030.

Kweleakwelea ni ndege vamizi anayeshambulia na kuharibu mazao kama mpunga, alizeti, na nafaka nyingine, hivyo kuhatarisha usalama wa chakula na kupunguza kipato cha wakulima. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, TPHPA kupitia wataalamu wake wa Kanda ya Mashariki imeweka mikakati madhubuti ya ufuatiliaji, tathmini, na udhibiti wa kweleakwelea kabla haijasababisha madhara makubwa mashambani.

Akizungumza katika banda la TPHPA kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Julius Nyerere  Morogoro, Dkt. Mahudu Sasamalo, Mkuu wa Kanda ya Mashariki, alieleza kuwa TPHPA imeendelea kudhibiti kwa mafanikio maeneo yaliyoathiriwa, ikiwemo Ifakara, Kilosa, Mvomero, na Bagamoyo, ambapo maelfu ya hekta zimeokolewa na mazao ya wakulima kuendelea kustawi.

“Kupitia juhudi hizi za kisayansi na kijamii, tunalenga kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanapata mazingira salama ya kilimo bila kutishiwa na visumbufu vya mimea. Hii ni sehemu ya azma ya Serikali ya kuhakikisha kilimo kinakuwa cha kisasa, chenye tija, na chenye mchango mkubwa katika pato la taifa,” alisema Dkt. Sasamalo.

Katika kuendeleza utekelezaji wa Agenda 10/30, inayolenga kuhakikisha kilimo kinachangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030, TPHPA inaendelea kuwekeza katika teknolojia, elimu kwa wakulima, na udhibiti endelevu wa visumbufu mashambani, ikiwemo matumizi ya mbinu rafiki kwa mazingira.

Wananchi na wadau wa kilimo mkoani Morogoro mnakaribishwa kutembelea banda la TPHPA kwenye Maonesho ya Nanenane ili kujifunza zaidi kuhusu mbinu za kisasa za kulinda afya ya mimea na mchango wa Mamlaka katika kuendeleza kilimo bora na biashara ya mazao nchini.

Share:

Friday, July 18, 2025

TPHPA Yachukua Hatua Kunusuru Ikolojia ya Ziwa Victoria Dhidi ya Gugu Maji

 














Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kupitia maabara zake za kisasa zilizopo katika Kituo cha Udhibiti wa Visumbufu vya Mimea Kibiolojia, Kibaha, mkoani Pwani, imeanza kuzalisha mdudu rafiki wa mazingira aina ya "mbawa kavu" (Cyrtobagous salviniae) kwa ajili ya kudhibiti gugu maji vamizi  (Salvinia molesta). Gugu hilo limekuwa tatizo kubwa katika Ziwa Victoria na vyanzo vingine vya maji hapa nchini, likisababisha athari kwa usafiri, mazingira, uchumi na maisha ya jamii zinazotegemea ziwa hilo.


Akizungumza wakati wa ukaguzi wa zoezi hilo, tarehe 18 Julai 2025, Mkurugenzu wa  Usalama wa Afya ya Mimea TPHPA, Dkt. Benignus Ngowi, amesema matumizi ya mdudu rafiki huyo ni sehemu ya mkakati endelevu wa kutumia mbinu za kibaiolojia kudhibiti visumbufu bila kuathiri mazingira. Alibainisha kuwa njia hiyo ni salama, rafiki kwa viumbe hai wengine na inaweza kusaidia kupunguza gharama kubwa zinazotumika katika kudhibiti magugu hayo.


Kwa upande wake, Ndugu Keneth Nyakunga, mtaalamu na afisa mwandamizi wa udhibiti wa visumbufu kwa njia ya kibaiolojia  alisema kuwa mdudu rafiki  huyo “mbawa kavu” (Cyrtobagous salviniae) waliletwa kwa ushirikiano na Serikali ya Uganda, ambako tayari wametumika kwa mafanikio makubwa nchini Uganda katika kudhibiti gugu maji vamizi (Salvinia molesta). Kwa upanda wa Tanzania  kwa sasa wapo katika hatua ya kumchunguza kwa kina tabia zake ikiwa ni pamoja na usalama wake katika mazingira pamoja na ufanisi na baadae kuwazalisha  kwa wingi kabla ya kuanza kuwasambaza katika maeneo yaliyoathirika zaidi na gugu hilo, ili kudhibiti tatizo hilo kwa ufanisi na kwa njia endelevu.

Share:
Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com